#EndPoliceKillings #EndEnforcedDisappearances

Nchi ya Kenya ina sifa nyingi za kipekee. Baadhi yake ni ubingwa katika mashindano ya riadha na vivutio maalum vya utalii. Hivi majuzi, Kenya iliandikisha historia kwa kuwa taifa la kwanza ulimwenguni kuzindua dawa ya kifua kikuu ya watoto inayoyeyuka majini na yenye ladha tamu. Hata hivyo, sifa hizi zimetiwa doa na msururu wa kashfa za ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Katika Kenya ya sasa, mauaji ya kiholela imekuwa  desturi ya maisha. Si nadra kusikia watu wametoweka katika njia za kutatanisha wasipatikane tena. Iwapo watapatikana, basi watakuwa wameuawa. Karibu kila wakati, tuhuma za mauaji haya hutupiwa idara ya usalama ambayo huzipuuzilia mbali kwa wepesi na kudai hazina msingi.
Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery amekuwa katika mstari wa mbele kuwatetea maafisa wa polisi na kuwaondolea lawama dhidi ya mauaji yanayokiuka sheria. Kulingana naye, kuhusika kwa maafisa wachache kwenye uhalifu haimaanishi kuwa kikosi kizima cha polisi ni dhalimu. Mtazamo huu wa kutoamini nazi mbovu huharibu zilizo nzuri umemfanya Nkaissery adaiwe kutia vibanzi machoni na pamba masikioni.

Waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Joseph Nkaissery

Waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Joseph Nkaissery

 
Katika mahojiano na Afisa Mkuu Mtendaji wa Africa Uncensored John-Allan Namu, msemaji wa polisi Charles Owino alikiri kuwa serikali ina uwezo wa kuwatowesha watu lakini haiwezi kufanya hivyo kwani hamna haja. Usemi wa Owino unaogofya hasa ikizingatiwa kuwa idadi ya watu waliouawa kiholela au kutoweka inazidi kuongezeka. Je, serikali inatumia kigezo gani kuamua iwapo kuna haja ya kuwatowesha au kutowatowesha watu?

Msemaji wa Polisi nchini Kenya Charles Owino

Mauaji ya Wakili Willie Kimani
Miezi michache iliyopita, wakili mtetezi wa haki za binadamu Willie Kimani aliuawa kinyama pamoja na mteja wake na dereva aliyekuwa akiwasafirisha. Kabla ya mauti yao, Kimani na wenzake walikuwa wanatoka mahakamani waliposimamishwa na kukamatwa na maafisa wa polisi. Hiyo ikawa mara yao ya mwisho kuonekana wakiwa hai.
Wiki moja baadaye, maiti zao zilipatikana kando ya mto Ol-Donyo Sabuk, kaunti ya Machakos. Uchunguzi wa daktari wa upasuaji ulionyesha kuwa waliteswa kabla ya kuuawa. Kilichofuatia ni maandamano ya halaiki yaliyohusisha mawakili na ambayo yalitikisa taifa nzima.

Mawakili na raia wakiandamana jijini Nairobi kufuatia kuuawa kwa wakili Willie Kimani. Kulia ni aliyekuwa Waziri wa Haki Martha Karua

Mteja wake Kimani kwa jina Josephat Mwendwa alikuwa amewasilisha kesi mahakamani akimshtaki afisa mmoja wa polisi kwa kumpiga risasi na kumjeruhi. Tayari, maafisa watatu wa polisi wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji hayo.
Kutoweka kwa watu eneo la Mlima Kenya
Katika uchunguzi wetu wa mauaji ya kiholela na kutoweka kwa watu, tulizungumza na wahasiriwa wengi kutoka sehemu tofauti nchini Kenya. Mmoja wao ni Lucy Wangui, mkaazi wa Solio eneo lililo pembeni mwa mlima Kenya. Ni eneo linalokaliwa na watu maskini waliofurushwa kutoka misitu ya mlima Kenya na Aberdares.
Tulikutana na Wangui wiki moja baada ya ukumbusho wa mwaka mmoja tangu kutoweka kwa mwanawe Patrick Maina. Kwa moyo mzito, Wangui alitusimulia jinsi Patrick alivyokuwa akimsaidia maishani. Kando na kumjengea nyumba, mwanawe alikuwa mfadhili mkubwa wa miradi yake ya kibiashara.
“Naona uchungu sana. Sikudhani mwanangu angepotea nisimwone tena,” Wangui alieleza, baina ya kwikwi za kilio. “Laiti ningelipata hata kidole chake nizike. Moyo wangu ungetulia…” Simulizi yake ilikatizwa mara kwa mara alipotua kupanguza machozi yaliyochuruzika mashavuni na kudondokea kifua chake.

Lucy Wangui ambaye mwanawe alitoweka mwaka wa 2015

Kulingana na Wangui, kustawi kibiashara kwa mwanawe huenda kulichangia kutoweka kwake. Anaamini mwanawe, aliyekuwa akifanya kazi ya ujenzi wa barabara, alitekwa nyara na maafisa wa huduma kwa wanyama pori na kuelekezwa kusikojulikana.
“Ukijenga nyumba nzuri au ununue gari, watu wa Kenya Wildlife Service hudhania wewe ni mwindaji haramu. Ukatili wao umefikia upeo.”        
Msemaji wa shirika la huduma kwa wanyama pori Paul Gathitu alikanusha vikali matamshi ya Wangui na kuwataka wanaotoa madai kama hayo wawasilishe ushahidi kwenye idara ya usalama.

Msemaji wa shirika la huduma kwa wanyama pori nchini Kenya Paul Gathitu
 
Uwindaji haramu
Kupungua kwa kasi kwa idadi ya ndovu nchini Kenya ni mojawapo ya sababu za serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wawindaji haramu. Hata hivyo, hatua hizi zimeishia kuwa mtego wa panya unaonasa waliomo na wasiokuwamo. Washukiwa wa uwindaji haramu wamegeuzwa mawindo.
Huenda hakuna anayeelewa ukweli kuhusu uhalisia huu kuliko John Kariuki, jirani yake Lucy Wangui. Aliponea mauti mapema mwaka jana wakati jaribio la kumteka nyara lilipotibuka. Ilikuwa usiku wa manane alipoamshwa na mngurumo wa gari lililokwama barabarani karibu na nyumba yake. Baada ya kitambo kifupi akasikia watu wakibisha mlangoni kwa fujo.
“Walijitambulisha kama polisi na kuniamrisha nifungue mlango. Nilipokataa, waliuvunja mlango na kujitoma ndani. Kwa maana sikujua wao ni kina nani, nilimshauri mke wangu apige nduru upesi,” Kariuki alitwambia.

John Kariuki akieleza jinsi maafisa wa shirika la huduma kwa wanyama pori walivyoweka bunduki nyumbani mwake na kumsingizia ni yake.

Mayowe ya mkewe yaliwavutia baadhi ya majirani waliotoka nje ya nyumba zao kushuhudia kilichokuwa kinaendelea. Kitendo hicho kiliwafanya wavamizi hao wasite kutekeleza lengo lao. Kariuki akawa amenusurika. Hapo kabla, alikuwa akisikia uvumi kuhusu maafisa wa huduma kwa wanyama pori kuvamia nyumba za watu na kuwatowesha wenyeji. Hakudhani uvumi huo ungegeuka uhalisia maishani mwake. Kwa muda huo wote, hakujua alikuwa mmoja wa waliokuwa wakiandamwa.
Punde si punde alishurutishwa na watu hao kutoka nje ya nyumba ili wafanye ukaguzi. Wakaingia kila sehemu ya nyumba yake wakipekuapekua hapa na pale.
“Walipokosa walichokuwa wanatafuta, mmoja wao alitoa bunduki kisiri na kuificha ndani ya kabati. Kwa bahati nzuri, mtoto wetu alimuona akifanya hivyo,” alitueleza Rose Wairimu, mkewe Kariuki.
Muda mfupi baadaye, Kariuki alitiwa mbaroni kwa tuhuma ya kumiliki bunduki kinyume cha sheria. Siku iliyofuatia, baadhi ya vyombo vya habari vilichapisha habari za kupatikana kwa bunduki hiyo.
“Polisi wanaamini kuwa bunduki hiyo ilitumika kuwinda wanyama katika eneo hilo,” gazeti moja nchini Kenya liliandika.
Tangu siku hiyo, Kariuki amekuwa akiishi kwa wasiwasi.
Vita dhidi ya ugaidi
Inaaminika na kudaiwa kuwa serikali inatumia vita dhidi ya ugaidi kama kisingizio cha kuwapoteza washukiwa wa ugaidi au hata kuwaua. Mojawapo ya visa vinavyohusishwa na hilo ni kutoweka kwa mfanyabiashara Hamza Mohammed mjini Garissa Februari mwaka jana. Picha tulizonazo za CCTV kutoka duka la Mpesa la Mohammed zinaonyesha akimhudumia mwanamke mmoja wakati wanaume wanne wanapoingia na kujifanya wateja.
Mmoja wao anafululiza hadi kwenye kaunta na kuanzisha mazungumzo na Mohammed. Wa pili anasalia mlangoni huku mwengine akiketi upande wa kushoto wa mlango. Wakati mazungumzo yanaendelea, mwanaume wa nne anaruka ghafla juu ya kaunta kwa usaidizi wa kiti na kumkamata Mohammed.
Tukio hilo linamtia wasiwasi mteja wa kike anayejaribu kutoroka lakini anazuiliwa na mwanamume aliye mlangoni. Baada ya sekunde chache, kamera ya CCTV iliyo nje ya duka inawanasa wanaume hao wakiondoka naye Mohammed huku wamemfunga mikono kwa nyuma. Inakisiwa kuwa wanaume hao walikuwa maafisa wa polisi kutoka kitengo cha General Service Unit.
Nduguye Mohammed aliiambia Tume ya Kitaifa ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya kuwa aliwapata watu hao wakimlazimisha Mohammed kuingia ndani ya gari aina ya Toyota Landcruiser.
“Alipokataa, mmoja wao alichomoa bastola na kutishia kumpiga risasi mdomoni,” alieleza.
Mohammed akawa hana budi ila kusalimu amri. Nduguye alipompigia simu baadaye na kuyafuatia mawimbi ya mawasiliano baina yao, aligundua kuwa Mohammed alikuwa katika makao makuu ya upelelezi wa jinai jijini Nairobi. Kufikia leo, Mohammed hajaonekana tena wala hajulikani alipo.
Kutoweka kwa Abdirazak Mohammed Haji
Kisa kingine kinamhusu Abdirazak Mohammed Haji anayedaiwa kutekwa na maafisa wa vikosi vya ulinzi vya Kenya kwenye kaunti ya Mandera. Mamake Haji, Awliyah Kerrow, anadai kuwa watu waliovalia magwanda ya kijeshi na kufunika nyuso zao walivamia eneo wanamoishi na kulazimisha watu kulala chini.
“Pindi tu walipomaliza kufanya ukaguzi, walimwendea mwanangu moja kwa moja na kumkamata. Walimpiga sana kabla ya kwenda naye,” alisema Bi Kerrow ambaye mpaka leo  hajamwona mwanawe.

Awliyah Kerrow, mamake Abdirazak Mohammed Haji. Haji inaaminika alitoweka akiwa mikononi mwa maafisa wa vikosi vya ulinzi wa Kenya.

Tuliiandikia Wizara ya Ulinzi tukitaka kuthibitisha madai ya kuhusika kwa maafisa wake katika kutoweka kwa Haji. Kupitia barua iliyotiwa saini na Luteni-Kanali Paul Njuguna, Wizara hiyo ilitujibu:
“Ni muhimu kuelewa wajibu na mamlaka ya vikosi vya ulinzi vya Kenya. Vikosi hivi huwa haviwakamati watu wala havina vituo vya kuwafungia raia. Kwa msingi huu, madai ya kuhusika kwa maafisa wake ni ya uongo.”
Mauaji ya Isnina Musa
Mbali na kisa cha Haji, vikosi vya ulinzi vya Kenya vinatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Isnina Musa Sheikh aliyepatikana Disemba mwaka jana katika kaburi la wazi eneo la Mandera. Wenyeji walishikilia kuwa Isnina kabla ya kutoweka alikamatwa na maafisa wa polisi na kuingizwa ndani ya gari aina ya probox. Walidai kwamba muda mfupi baadaye, gari la jeshi lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara liliondoka na kulifuata hilo la probox. Kwa mujibu ya ripoti ya daktari wa upasuaji, Bi Isnina aliyekuwa na umri wa miaka 32 alifariki dunia kutokana na pigo kubwa kichwani na kifuani.

Mwili wa Isnina Musa ukifukuliwa katika eneo la Omar Jillo, kaunti ya Mandera

 Akizungumzia mauaji hayo, Waziri Nkaissery alidai Isnina alikuwa akiwapikia wanamgambo wa Al-Shabaab kwenye kambi ya Bulla Hawa nchini Somalia kabla ya kutorokea Mandera.
“Pengine Al-Shabaab ndio waliomuua,” alisema Nkaissery.
Kugundulika kwa maiti ya Isnina kuliibua hofu miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu ya kuwepo kwa miili zaidi katika eneo hilo. Matokeo yakawa shinikizo nyingi za uchimbuaji ambao ulitekelezwa hatimaye katika eneo la Omar Jillo. Hata hivyo, shughuli hiyo haikuzaa matunda. Kufuatia kukosekana kwa miili zaidi, watetezi wa haki za binadamu pamoja na viongozi wa eneo hilo walifokewa na kutajwa kama waongo. Kwa wakati mmoja, Seneta wa Mandera Billow Kerrow aliyedai kuwepo kwa makaburi ya halaiki alipewa makataa ya saa 24 na Nkaissery kuomba msamaha au achukuliwe hatua kali. Kerrow akaungama. Ukurasa kuhusu kifo cha Asnina ukafungwa.
Ripoti za mashirika
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Independent Medico-Legal Unit, watu 126 waliuawa na polisi kati ya Januari na Disemba mwaka 2015. Miongoni mwa hao, 97 waliuawa kinyama huku asilimia 85 yao wakiwa wanaume. Idadi ya watu wanaouawa kama mende au kutoweka imesalia juu kwa miaka mingi licha ya idara ya usalama kukariri haihusiki kamwe.
Je, kuna uwezekano wa kuwepo kwa kikundi maalum cha maafisa wa usalama kinachotekeleza matukio haya? Ikiwa hakipo, inamaanisha mauaji haya na kutoweka kwa watu vinatekelezwa na wahalifu ambao ni raia wa kawaida? Lakini iwapo kipo, kwa nini kikaundwa na ilhali kuna sheria inayotoa mwongozo wa kuwaajibisha washukiwa wa uhalifu?
Katika Sehemu ya Pili na ya mwisho ya Kifo cha Mende, tutaangazia matukio zaidi na juhudi za familia za wahasiriwa za kutafuta haki.
Source: Africa Uncensored
Author: Dennis Mbae

SHARE WITH OTHERS

Share on facebook
Share on twitter
Share on whatsapp

SHARE WITH OTHERS

Share on facebook
Share on twitter
Share on whatsapp

GET INVOLVED

ONE

REPORT NOW

TWO

SIGN PETITION

THREE

FOLLOW TRIALS